Monday, February 12, 2007

Wetu ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa au wa kiunga?

Na Ally Saleh


Nilikuwa pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar wakati moja ya makundi yaliokuwa yanakwenda Makka yalipokua yakiondoka na nikaona hali ya vurugu ilivyo. Niliumia sana. Niliumia ndani ya roho.

Sikuamini hali inaweza kuwa mbaya kiasi hicho. Moyoni nilisema, laiti wakubwa wa nchi hii wangeliona…lakini kasha nikasema kwani hawaoni…sio wao wamepewa macho manne ikilinganishwa na yetu mawili?

Ilikuwa ni usiku, basi na mambo ndivyo yalivyozidi. Humjui aondokae wala humjui asindikizae. Palikuwa zahma-l-karadis. Hapana mipaka wala hapana pa kutoka na kuingilia, hapana pa kukalia wala pa kuvutia pumzi. Ilikuwa ni kitahanani kitupu.

Kwa sisi ambao hatujawahi kwenda Makka, ila tunaoona picha zake basi tukawa tunatania kwamba vurugu iliyokuwepo pale ni sawa na pale Waislamu wanapokuwa Saffa na Marwa au kumtupia jiwe shetani.

Maana kwa kweli ndivyo ilivyokuwa. Ila pale palikuwa njia haionekani na shetani wenyewe hakuwepo.

Sikutaka kabisa kufikiria wale mahujaji walikuwaje tukitilia maanani wengi ni watu wazima na hata hao vijana walikuwa na safari ndefu na bila ya shaka watakuwa wamechoshwa mambo ndio bado yaanze.

Ilibidi wenye nguvu zao wasukumane na watu na wabebe mizigo yao juu ya vichwa, na dhaifu kama mie ikawa ni kushikwa mkono kuongozwa kwa sababu kwa wao wenyewe tu, wasingeweza kufika kule mbele. Wangefikaje?

Najua sana vurugu hiyo ilichangiwa pia na waandaaji wa safari hizo za Hija kwa mipango yao isiokuwa minyoofu. Ila hilo kwa kweli si la leo, iko siku yake maalum ambapo tutalizungumzia.

Enhe, nilisema kwamba ilikuwa ni usiku basi tabaan palihitajika kuwepo mwanga. Wallahi, naapa kuwa hapakuwa na mbalamwezi wala taa ya umeme. Palikuwa hapana ulinzi na kwa hivyo ni pisha pisha na mwenye nguvu mpishe.

Hamu ya kuandika ikanijia pale pale, lakini nikasema na moyo wangu, " Punguza munkar," na hivyo ndivyo nilivyofanya. Nikasema, wacha litokee jengine basi hapo ndipo uandike maana utakuwa umefanya mambo mawili.

Kwanza lile la kuupa moyo subira, lakini la pili utapo pata jambo jengine utakuwa unaandika mambo yenye upana zaidi, maana hapo halitakuwa jambo moja lilokugharibisha kuandika juu ya Uwanja wa Kiamtaifa wa Zanzibar.

Naam, jina kubwa na kwa kweli linabeba sura nzima ya Zanzibar. Pale ndio ingilio au mlango wetu mkuu na ndipo wageni wanapoanza kutuona jinsi tulivyo. Ama itakuwa kujenga taswira nzuri au kujenga taswira mbaya. Hapana shaka sisi tungelipendelea hiyo ya tangulizi.

Haijachukua muda kupata kishawishi au isbabi ya kuandika kuhusu huo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, uwanja wetu wenyewe lakini ambao kwa dalili na ushahidi haupewi hadhi na haki inayostahiki.

Kwa maneno au matamshi ya kisiasa mtu aweza akatishika kuwa Uwanja huo unapata kila haja unayotaka lakini ziara za upelelezi za mara mbili tatu tu zitaweza kumfanya mtu yoyote agundue mambo kibao.

Mambo gani hayo kibao? Ni mambo ambayo mtu yoyote tu wa kawaida angeweza kufikiri au kuuwazia uwanja huo kama lingepatikana hili basi pale pangekuwa pazuri zaidi au huduma ingekuwa ni bora kuliko ilivyo hivi sasa.

Hatukatai kuwa uwanja wetu umejengwa katika mazingira ya kizamani, na kwa hivyo kwa sasa inaonekana vigumu kuongeza majengo na kwa hivyo nafasi ya kutenda kazi kwa nafasi zaidi.

Lakini hilo lazima lifanywe. Inabidi tutumie akili yoyote ile lakini nafasi ipatikane maana ukweli ni kuwa palivyo hivi sasa hapatoshi. Na kila uchao tukisema na kutaraji kupata wageni zaidi, kwa mfano watalii 150,000 kwa mwaka ina maana harakati nyingi zaidi pale uwanjani.

Hii ni mbali ya wasafiri wa ndani, ambao kwa sababu ya kuongezeka kipato na pia kukua kwa uchumi wa nchi, basi nao wasafiri wa ndani wameongeza sana.

Basi siku moja nikawa pale uwanjani siku ndege moja ya watalii ilipokuwa inakuja na nyengine ikiwa inaondoka, zote hizo ikawa ni kukutana hapa uwanjani petu. Na hapo ndipo utapoifaidi hali ya uwanja huo.

Hiyo ni mbali ya safari za kawaida za ndege zetu za hapa ndani ambazo kuruka na kutua kwake ni mashaka hayo ambayo nitayazungumzia, lakini ndio wao wafanye nini na fedha wanazoingiza katika mfuko wa Serikali pengine ni ndogo.

Lakini si chache hivyo maana safari hizo ni nyingi na wasafiri ni wengi na bila ya shaka haba na haba yao ya kodi ya kiwanja haikosi kuwa ni mamilioni, ambayo mtu angetegemea yangeelekezwa kiasi chake fulani kurudi ili kuimarisha kiwanja.

Kule kwenye madege hayo makubwa ya nje na ambayo wapandaji wake ndio tunaotaka kuwajengea taswira njema ndio usiseme. Midege hiyo mikubwa na mizito mpaka inachimba barabara ya kutulia na wageni wanatoa madola, mapauni na maeuro.

Mapesa yote wanayoyamwaga ndani ya nchi hii basi tunashindwa angalau kuwaweka katika kivuli wanapoondoka au kuwanusuru na mvua wakijipanga kuingia ndegeni.

Wengi wao naamini huwa wanauma meno na kujuta. Wakitaka kuja tena wanafikiri na adha ile ya uwanjani.

Mie sio katika wanaoamini kuwa hakuna la kufanya kuhusu uwanja wetu na kuwa tuinue mikono na kushukuru Walladhalina, Amina. Hapana yako mengi ya kufanya na yote ni ndani ya uwezo wetu, yaani uwezo wa serikali.

Kwanza kabisa ni kumpa uwezo wa kifedha meneja wa uwanja huo. Si rahisi kwa sisi wa tu wa nje, bila ya msaada wa takwimu kujua fedha zinazoingia uwanjani hapo kwa siku, kwa wiki na kwa mwezi.

Lakini tunaweza kufanya makisio kuwa si chini ya wenyeji 100 wanasafiri kwa siku na si chini ya wageni wastani wa 50 wanasafiri kwa kila siku ya Mwenyenzi Mungu. Mtu aweza kushangaa mbona idadi ya wenyeji na wageni yafanana au inakurubiana?

Hii naona ni kwa sababu idadi ya wageni wanaokuja nchini tumeambiwa mwaka uliopita ilipita 125,000 na bado inaongezeka na ukweli kuwa wengi wa wageni wa humu nchini ni wale amao wanaoingia kupitia uwanani hapo.

Haina haja ya kuzunguka na kujizonga isipokuwa kusema mamilioni yanayopatikana hapo yasiingie " katika mikoba ya ukili ya wafanyakazi tu" chembilecho Waziri Kiongozi, Shamsi Nahodha, bali asilimia 10 zirudi uwanjani ziweze kufanyiwa kazi.

Nasikia kilio hiki kimeliliwa sana . Kelele zimepigwa, lakini wapi. Na mie naamini hilo linatokea kwa mamlaka ya uwanja wa ndege, maana kuna mtu wa Mamlaka ya Mpato ya Zanzibar (ZRB) ameninong'oneza kuwa hata wao hawaipati asilimia 10 ya kile wanachokikusanya.

Kwa hivyo uwanja wa ndege ZRB na wengine kama hao hata iwapo wanakusanya malukuki lakini wakitaka matumizi huwalazimu waende kupiga hodi, kuomba na saa nyengine kupiga magoti.

Ndio maana taasisi hizi za serikali tunaziona nyonge nyonge na kwamba hazina ubunifu. Kumbe ukweli ni kuwa zina fikra mbali mbali lakini hazipati mapana ya utendaji kwa vile zina ukosefu mkubwa wa mtiririko wa fedha.

Kwa mfano naamini mamlaka ya uwanja wa ndege inaumia wasafiri wanapopigwa na jua au mvua wakisubiri kuondoka au hata wanapoingia. Hili linawakera ukiwatizama nyusoni mwao unaliona.

Wanaumia pia kuona uwanja wa ndege hakuna taa. Kukiwa na wasafiri wengi wa usiku kama nilivyoshuhudia kwa mahujaji basi ni tafrani tupu, na hili wasingependa liwepo, unajua ndani ya nyoyo zao.

Kwamba ipo haja ya kuweza kutenganisha wasafiri wa ndani na nje iwapo upo uwezekano, hilo pia wanalitaka. Wanajua ikiwezekana kuongeza jengo upande ule baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa, vurumai itapunguzwa sana upande huu. Lakini wafanye nini.

Tizama pale kwenye mapokezi wanavyobanana, tizama ofis za ndege za kukodi zinavyobanana, tizama eneo la kuwekea mizigo lilivyo dogo hivi sasa.

Fikiria sasa zimeingia ndege mbili za nje hali inakuwaje. Naambiwa inaweza kuchukua saa nzima tokea mgeni kufika mpaka kuondoka iwapo ndege mbili za nje zitaingia au kutua karibu karibu.

Najua kabisa kuwa mamlaka ya uwanja wa ndege inataka eneo liliopo mbele ya uwanja penye kiji mkahawa liwe sehemu ya uwanja ili pengine eneo la kuweka magari lisogezewe huko ili nafasi kubwa zaidi ipatikane.

Walivyo wabunifu wakiwa pesa unawaona hasa eneo la sasa la magari litaporomoshwa jengo au akili itatumiwa ili liweze kufaa kwa kazi mbili na sio kama ilivyo hivi sasa, kuwa ni kuegeshea magari, lakini pia halitoshi. Ndio yale ya mkia wa mbuzi.

Lakini fedha za uwanjani hapo si mkia wa mbuzi maana walioneemeka nazo, alhamdullilahi.

Nionavyo ni kuwa hata huduma za ndani ya uwanja hazilingani na hadhi ya uwanja huo.
S tunaingia bwana na kuona? Mbanano huwepo pale mpaka viyoyozi vyote vinazidiwa nguvu…wazungu tena hupata fursa za kukaa matumbo wazi.

Tunataka na hasa tunatamani tumnyonge meneja wa uwanja wa kushindwa kazi. Lakini tusimnyonge meneja au mamlaka ya uwanja kabla ya kutenda haki na haki ni kupewa asilimia 10, naam 10 tu ya wanayozalisha.

Uongozi upewe fursa zote halafu na sisi tuwe tuna haki ya kudai huduma bora na kamilifu. Au siyo bwana?

Iwapo watapewa ziada, hakuna ziada inayogomba. Hata hili pia lishindikane? Ndio pale wengine wakaona ipo haja ya kubinafsisha au kutoa mamlaka ya kishirika kwa mamlaka hayo ya uwanja wa ndege.

Siamini, siamini kuwa haiwezekani.

No comments: