Monday, February 12, 2007

Mechi za bar’za zastawi Zanzibar

Na Ally Saleh

Tabia ya kuzungumza katika ba’rza imeota mizizi sana Zanzibar. Ni jambo la kawaida mno kiasi ambacho imekuwa ni sehemu ya utamaduni wetu.

Na hii hapana shaka inatokana na ule utamaduni wa ujenzi wa kila nyumba ya Mswahili kuwa na bar’za, ila Waswahili wanaojenga mijengo ya kisasa aina ya kasri hilo sio tu halizingatiwi, lakini pia halina nafasi.

Karibu kila mtu ana bar’za yake ya mazungumzo. Na wengine huwa na zaidi ya bar’za moja na hii inatokana na kile anachokifuata katika bar’za moja ikilinganishwa na nyengine, au watu anaokutana na au pia wakati wa bar’za hizo.

Kuna bar’za kazi yake kuzungumza mambo ya dunia na siasa, wengine hukutana kuzungumza ushongo, wengine kucheza karata na bao na wengine michezo na mambo ya ujana.

Tabaan bar’za huwepo pia kwa mujibu wa umri au stahiki ya watu.

Tena mtu huchagua panapo mridhi yeye, ijapo pengine si mchangiaji ila ni msikilizaji, lakini almuradi na yeye ni mwanachama. Mtu huonekana kama mchawi hivi iwapo hana bar’za.

Wazanzibari hupoteza saa nyingi katika bar’za na wengine hata ndoa zao huingia matatani kwa vile wake zao wanashindwa kuwaamini ama kwa tabia ya kukaa muda mwingi humo vibarazani au kwa kujua ushawishi na ubilisi uliomo humo vibarazani. Si imesemwa bilisi wa mtu ni mtu?

Si ajabu wageni wakawa wanapata hisia kuwa Wazanzibari ni wavivu, ingawa watu wenye nadhari na kazi zao hasa hawakai barazani…mpaka wakati huo ambao kazi zao zimemaliza, maana kazi na dawa.

Zamani bar’za zilikuwa hazina majina. Sana labda hutajwa mtu maarufu anaezungumza pale, kwa mfano “ Bar’za ya Maalim Said” na kadhalika. Lakini leo au tuseme kuanzia miaka 25 iliyopita kila bar’za ina jina.

Inaweza kuwa jina lenye staha kama Right Brothers au lenye amani kama Peace. Inaweza kuwa la miji au nchi za kigeni kama Durban au Lebanon na majina mengine mengi ya ajabu ajabu.

Najua zamani zaidi majina ya bar’za yalikuwepo kama vile Comeback, ambayo ilikuwa ikisifika sana kwa mambo ya ujana, lakini hakikuwa kitu kilichoenea sana.

Kama nakumbuka uzuri majina kwenye bar’za, kwa mtindo tulonao sasa, yalianza kuja pale ujana nao ulipoanza kustawi na mtindo wa kufanya party ulipopamba moto. Kila bar’za ilitaka ijitambulishe vilivyo

Lakini pia zamani hiyo ba’rza zilikuwa hazijapewa jina la kuitwa maskani. Nionavyo neno maskani kuitwa baraza ina maana ya kujitambulisha kwamba wapo pale kwa muda mrefu zaidi au kwa kudumu.

Hii ina maana zaidi ya kuwa kwa kuwa hawana kazi basi mazungmzo na makaazi yao ni hapo na hivyo hayo ndio mas’kani yao.

Ushindani wa soka baina ya bar’za kwa mtindo tunao uona hivi sasa ulizuka kiasi cha miongo miwili hivi. Hapo ndipo kila aina ya michuano ikaanzishwa na vijana kushirii kwa hamasa zote.

Nafikiri mechi za bar’za zilianza kupata nguvu pale kiwango cha soka cha Zanzibar na usimamizi mzima wa mchezo huo ulipoanza kutetereka. Washabiki wakaanza kukosa raha, na wachezaji kuvunjika moyo na kwa hivyo ikawa lazima kupata mbadala.

Nakumbuka viongozi wa vilabu walipoanza kukasirishwa na wachezaji wao kushiriki mechi hizo za bar’za kiasi ambacho walikuwa wakichukua hatua za kuwafungia wachezaji, lakini haikusaidia kitu.

Ilianza kuonekana kwamba wachezaji walizipenda sana ligi hizo za bar’za na kuwazuia wachezaji au kuwatia adabu isingesaidia kitu, na badala yake viongozi hao hao wakaanza kuzitumia ligi hizo kutizama vipaji vipya ambavyo vimeshindwa kujitokeza katika mechi za kawaida za ligi.

Ndipo kwanza mechi za mwezi wa Ramadhan ziliopoanza kuchipua. Viwanja vya Malindi, Mnazimmoja na baadae sehemu za Nga’mbo zikazuka ligi za ushindani wa Ramadhan. Vyovyote iwavyo mpaka sasa ligi inayoandaliwa na Dula Sunday ndio inakuwa bora kabisa.

Inashangaza kijana huyo anavyoweza kusimamia mashindano yote karibu peke yake na michuano kuweza kuanza na kumalizika. Amejijengea heshima kubwa miongoni mwa vijana.

Sasa umekuwa utamaduni mkubwa kuwa na mashindano wakati wa Ramadhan na fainali yake kufanyika yaumu shaka, yaani siku ya kutarajia mwezi kuundama.

Ligi za ba’rza zina raha sana na hupata watu wengi kuliko mashindano ya ligi ambayo huandaliwa na Chama cha Soka Zanzibar ZFA. Ligi za bar’za pia zina msisimko kuliko mechi zinazoandaliwa na ZFA.

Tizama hamasa ya wachezaji na namna wanavyojitolea kulinda majina ya bar’za zao…ni kuliko wachezaji katika ligi ya soka ya kawaida. Tizama jinsi ya washabiki wanavyojipamba na kushangiria…kuliko washabiki katika ligi ya kawaida.

Tizama usimamizi wa ligi na uchezeshaji…ni kuliko wa mashindano rasmi…tizama ahadi za utoaji wa zawadi…inatimizwa ikilinganishwa na michuano rasmi ambapo washindi hawapewi vikombe.

Kwa kuwa michuano hii huchezwa kindavandava, basi hapa ndipo pahala pazuri sana kuweza kujua uwezo wa mchezaji…maana hakuna anaejilegeza..kujilegeza ni dhambi maana sio tu kuwa utachekwa lakini utaifungisha timu yako.

Hapa pia ni pahala pazuri pa kuona vipaji au uwezo wa mchezaji. Binafsi timu yangu imefaidika mara kadhaa kupata wachezaji kwenye mechi za bar’za au kuona uwezo halisi wa mchezaji kwenye mechi kama hizi.

Uzuri mwengine wa mechi hizi ni nafasi ya wachezaji wasio na namba au nafasi katika klabu zao au wanaotafuta soko kuweza kuonekana.

Jengine ninalolipenda kwenye michuano hii ya bar’za ni ile hali ya wachezaji maarufu kuweza kuchanganyika na wale wachanga na wasio na uzoefu ili sio tu kujisikia wamecheza nao lakini pia kuwapa moyo kwa kucheza nao.

Hii ni muhimu mno, maana huwa ina mjenga vyema yule chipukizi, hasa kwa vile mechi hizi huhudhuriwa na watu wengi sana.

La mwisho linalofanya nihusudu mechi hizi za bar’za ni ile hali ya kuwa mpira unarudishwa kwa wapenzi. Maana mpira ni wapenzi, sasa ikiwa unachezwa bila ya wapenzi hata uwe mtamu vipi au kwenye kiwanja kitamu kama halua, huwa haina maana yoyote.

Mechi za bar’za raha yake kubwa ni wapenzi. Na mimi naamini si kwa sababu mechi hizi huwa bure au kwenye viwanja vya wazi ndio maana zinahudhuriwa na watu wengi, si sababu kabisa.

Nionavyo washabiki wanajaa kwa sababu mechi hizo zina hamasa, kiwango cha juu cha soka kinaonekana, maandalizi na usimamizi wake ni mzuri, fursa ya kuwaona mtaani wachezaji nyota na kutimizwa kwa ahadi za zawadi…kama ni kikombe kinatolewa, kama ni fedha zinatolewa la kama ni n’gombe basi pia huletwa uwanjani akakabidhiwa mshindi kama hivi majuzi walivyopewa bar’za ya Lebanon baada ya kuwalaza Durban.

1 comment:

Abu Ammaar said...

Jazaaka llahu khayraa sh kwa kutukumbusha mechi za barza ila tu zimeleta tabia moja ambayo huathiri mwenendo mzima wa lengo na madhumuni ya Ramadhaan. Mwezi wa ibada, mwezi wa rehma na mwezi wa kuachiwa huru na moto.Nakumbuka mimi mwenyewe nilikuwa mshabiki mkubwa enzi hizo lakini leo nnaweza kusema kwamba zimeathiri sana kuweza ya kufikia malengo halisi ya funga.

Muda huu wa jioni ni muda wa kubaki misikitini kusikiliza darsa lakini vijana huutumia kwa kushindana katika mashindano yasiyokusudiwa kwa mwezi huu. mashindano ya Quraan, ibada,kusoma masomo ya dini ni mashindano halisi ya kuyajengea utamaduni katika mwezi mtukufu.

Wajazaakumu llah