Thursday, February 22, 2007

Nabwa umetuwachia kalamu

Na Ally Saleh

Hatua yake ya kwanza
Akifika kaburini
Mimi hilo ndani naliamini
Ni Ali Nabwa kuuliza
Jee huku nilikoletwa
Lipo gazeti niandike?

Hakuna hapa gazeti
Ataambiwa na karipio kupewa
Sharubu za Munkar akikaziwa
Wewe vipi, kwanza hapa zoea
Makazi yako ya kudumu
Ndipo mengine uulize
Tuanze na takadumu?

Nipeni niandike makala zangu
Duniani kule ambazo
Sikuwahi kuzimaliza
Maana uhai nimekatizwa
Nikiwa nina mengi umma kueleza
Uss!! Ataambiwa

Hiyo ndivyo atakavyokuwa
Mwenzetu huyu alotangulia
Alietuachia sisi ukiwa
Ukiwa wa habari na taarifa
Kiza…kiza hata kupapasa hatuwezi
Wengine ndio kwanza maziwa
Ametuachisha…kunyonya uwezo wake

Ghafla taa imezimika
Tukiwa katika meza
Mbele ya kompyuta yetu
Tukiandika habari… kujuvya umma
Na yeye kinara wetu
Akididimiza kalamu yake
Kuandika sisi tusiyoyajua

Aliandika mengi mno
Mengi ya kujaza dunia
Kama ingekuwa ni karatasi
Ya ndani mno
Kuumiza moyo
Kama ingekuwa unayafika
Lakini maandishi yake
Ukuta yaligonga
Masikio yakapita…tundu hadi tundu

Nabwa kalamu yake haijakauka
Ila mkono tu umesita kuandika
Maana mwenye uhai ametaka
Kiumbe chake kukichukua
Aliyetua ndie amechukua
Na sote kwake tutarejeya

Kinachotuuma si kifo
Maana kifo ni wajibu
Wajibu mchungu lakini
Kuuweza kukwepa haiwezekani
Ila kinachotuuma ni namna
Mwenzetu huyu alivyoondoka
Kalamu ikiwa na wino

Mengi alitaka kuandika
Umma wetu kuuamsha
Kujua yaliopita mwetu
Humu nchini wengine
Watakao kuwa yafunikwe
Ala! Haiwezekani, ndipo akajitolea

Na huko kujitolea
Ndiko kuliko mchongea
Alikuwa shujaa, lakini shujaa akanaswa
Kwenye mtego wa maadui zake
Jarife likamtanda, kidole hakipenyi
Ilikuwaje wewe karambisi ukawemo
Ndani ya kundi la tasi?

Papatuzi…na pirika wapi zimfikishe
Wenye nguvu na ulwa yao wataka
Wayafiche hadharani yasitoke
Na hilo Nabwa lilimuuma
Alisema hatakufa, katu hatakufa bila kusema
Kutapikia sandani hata kukiri.

Walopenda na wasopenda
Makala zake walisoma…wakacheka
Wale walotenda
Wengine wakalia…kwa kwikwi
Wale walotendewa
Wengine wakasema sasa iwe nini
Wengine wakasema: Sema Nabwa sema
Magazeti yakanunuliwa…Nabwa kasema

Naam, Nabwa alisema lakini
Sauti ilisikika…masikio ilipenya?
Hisia zilipatikana?
Yaguju…roho ngumu, kalbi kasi ikawa
Ndipo akatumbuka maradhi
Kuhojiwa yeye karambisi
Vyereje kwenye kundi la tasi?

Nabwa hatupewa gazeti huko aliko
Atapata hukumu kwa alichochuma
Miaka aliyokaa duniani
Lakini kama atapewa huruma
Basi itakuwa angalau waliotendewa
Yeye kuwasemea…
Alipokuwa na kalamu

Gazeti ameliacha duniani
Ambako hakuna mtu kama yeye
Aliyeweza kuwa ni taasisi
Taasisi iliyotimilia na inayoweza
Kupigana na serikali hadi kifo
Maana mapambano yalikuwa ni
Nabwa na Serikali
Nabwa na Serikali
Nabwa na Serikali

Sasa ufwe…
Amepumzika
Amelala
Amekwenda
Amefika
Serikali inae kwa kupambana nae?

Wino upo maana kalamu haijakauka
Lakini mkono wa kushika kalamu upo
Sijui…
Maana shujaa huwa mmoja tu
Wengine huwa ni waigizaji
Na serikali hupambana na shujaa

Sisi si mashujaa, si mashujaa kama yeye
Ila kalamu tutaichukua
Hatutandika kama yeye
Lakini juu ya kaburi lake tutapanda mche
Ambao tutautilia maji na kuupalilia
Ili tuweze bado kuwa na mawasiliano nae
Maana kuandika bado tunataka
Na yeye ameondoka na kila kitu
Kalamu tu aliyotuachia haitoshi
Nabwa…hakutuachia mengi…
Mengi umeondoka nayo…

Lala salama
Usiulize gazeti maana hutapewa
Usiulize kalamu maana huko haiku
Sisi tutakuwa na gazeti na kalamu
Kama unatusikia…
Kama unatusikia…tupe vitu
Tutaandika…naam… tutaandika

No comments: