Monday, February 12, 2007

Happy Birthday CCM, mwana usiyejua shida!


Na Ally Saleh


Hongera Chama cha Mapinduzi!!! Hongera ndugu yetu, wengine mwanetu na wengine mjukuu wetu. Vyovyote iwavyo, hongera haigombi. Happy Birthday CCM….tunakutakia siku njema ya mauled.

Mungu akuweke uishi miaka mia, na uende kwa mkongojo!!! Siwezi kuwa hiana mpaka nikatae kukutakia maisha marefu ingawa sina hakika kuwa wewe ndugu yetu unaweza kuwatakia wafanana na wewe maisha marefu.

Tunakupa hongera kwa mengi, mengi sana. Maana mwenzetu umepita siku na miaka mpaka leo nchi nzima inatikisika ikiimba sifa zako na kusherehekea kuzaliwa kwako. Dogo hilo?

Si dogo maana birthday za wengine hawapati fursa ya kutengenezewa fulana wakagaiwa wala mishumaa ya kupuliza kwenye keki, seuze ngoma na chereko.

Leo unatimiza umri wa miaka 30 kutokana na kuzaliwa kwako tarehe kama ya leo, yaani Februari 5, 1977. Si haba kuwa mpaka leo upo na tunakuona, mzima wa afya. Na umejaa tele kama pishi ya mchele.

Hujatetereka, pengine umetikiswa hapa na pale, basi. Lakini wakati wewe umetikiswa wenzio wamepatwa na matetemeko ya ardhi na wengine wamefunikwa na vifusi siku sio zao.

Hospitali uliyozaliwa, maana ulibahatika wengine huzaliwa majumbani, bado ipo pale pale lakini iko hali mbaya kiasi ambacho nasikia masahiba wako na waliokuwa wa wazee wako wanataka kuja kuitengeneza.

Inasikitisha kuwa kijana muelewa, mwenye uwezo kama wewe ukapadharau pahala ulipozaliwa kufikia hali ilivyo sasa. Lakini ndiyvo mlivyo vijana wa siku hizi, nyote jora moja ila mishono tu tofauti.

Baya ni kuwa karibu kila mwaka umepatumia pahala hapo mara kadhaa, lakini hata kuruzuku maji basi, au brashi ya rangi? Sakafu yake hivi sasa aibu kuhusishwa na weye.

Nina hakika unaringa ukijitizama hapo ulipo. Mrefu kama twiga, mkali kama simba, mnene kama mbuyu, miraba minne kama kifaru na mjanja kama sungura. Ukizitizama sifa hizo, unajiona wewe ndio weye. Ulipo hutachechetuka, wengine wote sisimizi tu kwako.

Unajiona mtimilifu, mpatifu na mzoefu. Hakuna kama wewe, hilo sisi tulokuona ukizaliwa tukikutizama usoni tu tunakuona. Tunaona sijui ndio tambo au majisifu au jeuri, lakini usikatae bwana hilo unalo. Pengine mwenye huoni hiyo ni ila, maana kawaida huwa desturi.

Ni mkamilifu kwa maana ya kukamilia kimuundo, kisera na kimkakati. Maana wewe una mashina nchi nzima na umeota mizizi; sera zako ndizo zilizosikilizana zaidi na watu kuzichagua na kimkaati nani akuwezae…nyumba hadi nyumba na “mvungu hadi mvungu”, chembilecho mama Salma Kikwete.

Ambacho nina hakika nacho pia katika hilo suala la mikakati, basi magodoro pia yalifunuliwa, maana ndio maana mpaka leo usufi umetanda mitaani na wengine ukitusumbua katika uvutaji pumzi.

Hata mwenyewe hupumuwi kwa raha, lakini kama desturi yako unakataa kukiri na unasema hakuna usufi hapa, mbona wewe huoni wakati unaukupua na tunauona umekuganda kwenye kope zako kiasi cha kukuziba macho.

Ni mpatifu maana fedha haikupigi chenga, majimbo ndio usiseme na serikali unazo kibindoni. Kampuni za mafuta zinajipendekeza kwako, za simu zinalala kwako na hazina ya Serikali ufunguo unao wewe kibindoni, kama Baniani Kamba.

Na ni mzoefu kwa mbinu na hila na ndio ukafika hapa. Ndio maana kampeni zako hazina ukwasi. Maburunguta nje nje, mafuta ya petroli chekwa na misosi na moto wa kukanzia ngoma huwa ni vitu visokosekana.

Nchi hii imeshuhudia vifo vingi sana vya watoto kama wewe. Wengine wamekufa uchangani, wengine wamekufa balegheni na wengine wamekufa wakiwa vijana shababi, ambao wengine walikuwa wameshaanza kuwatumainia.

Mlozaliwa wakati mmoja wengine wamekufa kwa utapia mlo, wengine wamepopotoka kwa polio na wengine wamekuwa punguani. Kama nakumbuka uzuri wewe ulikuwa ni mtoto peke yake uliozaliwa na wazazi wawili – Afro Shirazi na TANU.

Mamaako tuliambiwa ni Afro Shirazi na babako TANU. Lakini sote tulikuwa hatujui kuwa Afro alikuwa mwanamke, maana muda mrefu hapa kwetu Zanzibar tulijua ni mwanamme, wallahi naapa au kama kiapo cha kwetu Pemba, baraatu nakualfia na mama yangu

Udume wa Afro Shirazi tuliushuhudia alipowatwanga makonde vijana wenziwe akina Umma Party pamoja na kuwa kama Cassius Clay kwa mbwembwe. Pia Afro akambwaga ZNP aliyekuwa kama Rocky Masiano na mwisho Afro akamgaragisha ZPPP ambaye alionekana kama Sony Liston wakati huo.

Lakini ghafla siku ile unazaliwa tukasikia kuwa Afro ni mama. Tukaona haya makubwa lakini hatujayauliza, maana mambo ya nyumba kunga. Sasa leo mwenyewe umekuwa mkubwa na mdadisi unaweza ukayauliza. Yalikwendaje, hata Afro akawa mama…na umama huo unaendelea hadi leo?

Umeishi mpaka ulipo hujapata utapio mlo maana umezaliwa katika familia yenye kipato kwa hivyo vyakula vya protini, wanga na mafuta vimekuwa haviadimiki kwenu, chokoleti na matunda hayo ndio usisime. Kuhusu ma apple ndio usiseme, mpaka Kwamtipura yamefika.

Maisha ya shida hujayajui kabisa, wewe unayasikia tu kama matangazo ya redio. Ukosefu huujui kabisa maana hujawahi kulala na njaa, sio kama wengine waliowahi kulala kwa uchochoni, mabiye au boribo.

Zamani kidogo wapo walioponea kwa unga wa manjano wa sembe ambao tuliambiwa ni chakula cha farasi Ulaya au zaidi Marekani…nay ale maharage ya ajabu ambayo mara yalikuwa manjano, mara kahawia na mara zambarau.

Wakati ule wa foleni za vyakula na kwenye mabekari…wewe kabisa sijawahi kukuona katika kesha na timbwa za wakati huo. Wenzetu wa kike na kiume walibakwa na kunajisiwa, mama zetu walifunuliwa nguo zao kwa ajili yetu, lakini wewe na familia yenu hamkuyajua hayo.

Tuseme kwa ujumla umezaliwa katika nyumba kubwa yenye fursa na satwa. Yenye ulwa na stahiki zote.Umelelewa kwa vitanga na mbeleko. Mpaka leo, nyumba yenu ndio kubwa kiamboni kote, ijapokuwa haijaongezeka kitu, kubwa baraka ya kuzongwa na msitu.

Halafu ulipochuchuka tu ukaanza ukorofi. Ukasema jahara kuwa pasiwepo na mwanamme yoyote ule ambae atakuzidi wewe. Wewe ndio wewe uwe kama jogoo la mtaa yaani makoo yote uyazalishe wewe, chembilecho wenzetu wewe ndio “ dume la mbegu.”

Kwa hali hio ukakataa mtu yoyote asijenge nyumba wala asipande mti. Maana nyumba na mti ni dalili ya uhai, na wewe ulikuwa peke yako, kama ulivyojinata ndie mwenye uwezo wa kuhuisha na kufisha.

La, sikufuru. Leo ndio unasema kuwa nakufuru. Hayo uliyasema bwana, usinisute.

Si tuliambiwa kuwa CCM imeshika hatamu. Labda hatamu za lijamu za kumpinda n’gombe utakavyo bila ya kujali maumivu kwenye pua zake, machofu na njaa yake au pia kuchagua atakako kuenda.

Na kwa kweli sisi wakati huo wa pawari za CCM, hatukuwa kama ng’ombe bali tulikuwa kama punda tena yule wa Mwembemakumbi au wa pale Amani. Bakora nyingi, mtama na maji kidogo.

Tuliambiwa lazima kuwa CCM. Ukitaka kazi, masomo, matembezi na chochote kile. Lakini pamoja na lazima yote akina sisi wengine tulikataliwa uanachama kabisa kabisa. Mpaka leo tukijiuliza hatupati jawabu.

Sote tulitakiwa tuwe chama kimoja, kama kibla. Tukubali itikadi kama Kurani, na tuwe chini ya mawazo na fikra za Mwenyekiti mmoja. Tuwe waladhalina amina au wasamiina wawataana. Tuwe kama matoto ya reli, tuvutwe na kubururwa.

Pengine kutakuwa na hoja hayo ni ya wakati ule. Lakini wakati ule,na mimi nitauliza , kulikuwa hakuna nchi ambazo zililkuwa na vyama vingi na watu wake kuwa na uhuru wa vyama wavitakavyo? Hicho kisiwe kisingizio.

Tukubali tu kuwa ulikuwa unataka upate utawala wa kujifaragua. Ulianza mapema kupata makole ya wazee wako TANU na ASP ambao na wao walianza mchezo huo mapema kabisa.

Na kosa hilo ndio lilozua utata katika siasa za nchi hii hadi leo. Maana ASP ilipokataa vyama vyengine ilikumbatia watu waliokuwa wanachama wake au wapenzi wake na hao wakapewa nafasi zote kushika…walizoziweza na wasizosiweza.

Nchi ndipo ilipoanza kwenda songombingo. Maana kukaanza kuwa na makundi ya wenye haki na wasiokuwa na haki. Wenye haki ni wale ambao walikuwa na uhusiano na ASP na wengine hata ambao hawakuwa ZNP, Umma wala ZPPP wakati wa kwenye kapu moja… kama hukuipenda ASP, na tabaan CCM basi wewe ni hao hao…

Na leo ukitimiza miaka 30, bado CCM umo kwenye mawazo mgando kuwa wengine wote ambao si wanachama wa CCM basi ni akina hao hao ukisahau kuwa muda nao umesonga na mambo yamebadilika sana.

Unajisifu siasa za vyama vingi umezileta wewe…lakini la ajabu umeshindwa kukubali kuwa maadamu vyama vyengine vipo basi tabaan vina haki na nafasi ya kushika madaraka. Sio wewe tu ndio mwenye uwezo, la.

Sasa na hivi leo tumekuwa na hiari kubwa. Hiari ya kupenda na hilo likiambatana na kuchaguwa. Kupenda ni chama mtu akipendacho na wananchi wote wawe na haki ya usawa ya kuchagua chama kinachomkuna roho yake.

Hiari kubwa ya kukipigia kura chama akipendacho na kukitakia uwezo wa kuingia madarakani…na kuwa madaraka sio tu suala la kupishana bali ni matokeo ya matakwa ya umma.

Kuwa kuchagua kwa leo si kutumia nguvu. Si kuwafanya polisi na majeshi waunge mkono kwa lazima chama tawala, si kuipinda mkono Tume ya Uchaguzi na wala si kuwa na vikosi vya vijana wasioambilika.

CCM ijue usimamizi wa nchi ni wa wananchi. Weusi wana haki na weupe wana haki. Wa Magharibi wana haki na wa Kusini wana haki. Sivyo kama tuonavyo.

Maadam leo unasherehekea siku yako ya kuzaliwa ujue na ujikumbushe kuwa pia kuna mauti. Si vizuri kutakabar maana kifo kinaweza kuwa ni kibaya sana.
Lakini bora nisiiharibu siku kwa kutishana kwa vifo maana kwa nikuonavyo naona wewe CCM huamini kabisa kama utakufa. Unaona kuwa umeumbwa uishi milele, maana usingefanya uyafanyayo kama ni vyenginevyo.

Ya kufa yako mbali, maana ni majaaliwa na siri ya Mungu lakini naona siku ya kuukosa huu ulwa ulonao tu basi unaweza ukafa kihoro, audhbillahi mindhalika.

Hongera CCM kutimia miaka 30!!!

No comments: