Tuesday, March 20, 2007

Umma Usiposimama!!!

Wajinga ndio waliwao
Waswahili walisema…
Sijui kama huo msemo
Wanao…maana mimi
Siku nyingi duniani nimehama
Na yalioko huko sinayo
Na ndipo wafanyao
Wanapovinjari na jeuri
Wengineo wanatizama
Wanyonge na wamekosa ari
Kwa vitendo na zao kalima
Mapuuza…wakifanya
Si letu?
Wengineo huo wasema
Letu sote basi nalitote
Umma hausemi
Maana kwa ujinga
Husema…kifo cha jamaa…

Duniani mimi nilipokuwa
Pumzi zangu nikipumua
Na kalamu ikiandika
Hilo nililikataa
La muhogo wetu wa jahazi
Misumeno kuukerezi…
La ila hilo!!!
Tobo dogo likianza
Wenye kasi wataenda
Kwa ndege na helikopta
Na boti zao za kasi
Akina nyinyi kuwasaza
Mzame na muhogo wenu
Wao hao…
Wandoka na vyenu
Vyenu walivyokusanya
Na nyinyi kimya mukinyamaa
Ilhali mnaona…uhaini mkubwa

Nilipokuwa Kikwajuni naishi
Mengi mno niliandisi
Hivi kweli hii ni hali halisi
Ya umma
Umma wetu wa watu
Kuuduna
Usiseme
Unyamaze
Wakati unaona hivi hivi
Mtu anajipimia ndani
Ya hifadhi ya karne
Kikataa
A sijui ploti
Kwa uroho wa nafsi
Anaua …yuko tayari
Kuua historia…uhaini mkubwa
Na umma hausemi
Kimya umenyamaza
Hili hata huku niliko
Linaniumiza japo mifupa mitupu


Yale ya langu jicho
Na upande wa sikio
Hayafai
Maana yangekuwa yanafaa
Kama wangekuwa na haya
Au kuona vibaya
Kufikiria wengine…
Mnakula sahani moja
Keshafika upande wako
Anarambaramba
Na wewe unasema
Lako jicho na kidole
Jicho watalitofua
Sikio watalidumua
Na kidole watakikwapua
Kwani hilo la ajabu
Au siri?
Wana roho ngapi
Mwao mikononi walizohujumu
Na haiwashughulishi

Umma lazima useme
Maana mtango unatambaa
Kama ulikuwa masafa
Sasa ujuu yapaa
Na jua litakapotua
Jua la umri wa mamlaka
Kila kitu wamekokozoa
…Yasije yakawa yale ya
Mchezo wa kitoto
Wa nyoka…
Mara keshafika kwako
Unamezwa kwa dakika
Kama hukuwako

Umma lazima useme
Maana akilini nionavyo
Haiingii
Kwa mchezaji kunyongwa
Sababu ya picha yake
Lakini…
Mpiga picha kuonywa
Kwa picha ya mchezaji
Huyo huyo…
Wakati uchi ni ule ule…
Na staha ni ile ile
Na maadili ni yale yale
Mnakwenda wapi nyie waja wa
Dunia mie niliyoiacha

Umma lazima useme
Kwa mkubwa kutania
Maisha ya watu kuchezea
Kwamba “ Maradhi tumeondowa…”
Na watu wakeugua
Na maisha yakepotea
Na kwamba wanamtafuta
Mgonjwa wa dawa
Hata rupia tayari kutoa
…Hakika dharau imekuwa
Ila umma wenu…haya
Waona, wayaona
Ni ya kawaida…
Nguvu ya kuuliza, kuhoji
Imepotea…arijojo
Imekwenda …kama nilivyokwenda
Mimi…


Umma useme leo
Unapoweza kusema
Ujipe nguvu ya kunena
Ungojeapo kesho
Hapatakuwa kalima
Kalima ni leo
Leo ni kalmia
Ya watu ambao
Vya chukuliwa vyao
Zachezewa staha zao
Na hufanyiwa mzaha
Maisha yao
Umma usiposema….

Ally Saleh
Machi 12, 2007

1 comment:

Rashid Mkwinda said...

Wapo walosimama na kjiona kama wako hima, bali waishi kwa kutetema na kujawa nma dhulma, iwapi yao nia njema ilhali dunia si njema na wala si mahala pema?

Nia ni njema bali matumaini si mema, walao hula wima bila kunawa tena kwa kukomba nakusaza makombo kwa yatima ambao hudiriki mlo mmoja wa chakula kiso chema.

Hula kwa kujaza matumbo na kutafakari maisha magumu na machungu, siku hizo zenda mbele na katu hazirudi nyuma.

Wako wapi watu wema waliotajwa kwa majina na utukufu wakatukuta nasi tukawawekea kumbukizi njema?

Wako wapi wafalme walikokula wao na kuwaacha vijakazi wakila makombo na matumbo kuwauma?

Wako wapi wajane wahanga ambao waume zao wamehajiri ama kuuliwa bila sababu za kina na kuziacha familia roho zao zinauma?

Wawapi hao watwana walotawala kwa mabavu na kudiriki kubaka vigori vilo ndani kisa hamasa za kisiasa ilhali nasi macho yetu yanaona?

Tupige mbiu kukataza maovu na waovu watokomee ili nia iwe ni kuongozwa na watu wema.

Wakatabahu