Tuesday, March 20, 2007

Umma Usiposimama!!!

Wajinga ndio waliwao
Waswahili walisema…
Sijui kama huo msemo
Wanao…maana mimi
Siku nyingi duniani nimehama
Na yalioko huko sinayo
Na ndipo wafanyao
Wanapovinjari na jeuri
Wengineo wanatizama
Wanyonge na wamekosa ari
Kwa vitendo na zao kalima
Mapuuza…wakifanya
Si letu?
Wengineo huo wasema
Letu sote basi nalitote
Umma hausemi
Maana kwa ujinga
Husema…kifo cha jamaa…

Duniani mimi nilipokuwa
Pumzi zangu nikipumua
Na kalamu ikiandika
Hilo nililikataa
La muhogo wetu wa jahazi
Misumeno kuukerezi…
La ila hilo!!!
Tobo dogo likianza
Wenye kasi wataenda
Kwa ndege na helikopta
Na boti zao za kasi
Akina nyinyi kuwasaza
Mzame na muhogo wenu
Wao hao…
Wandoka na vyenu
Vyenu walivyokusanya
Na nyinyi kimya mukinyamaa
Ilhali mnaona…uhaini mkubwa

Nilipokuwa Kikwajuni naishi
Mengi mno niliandisi
Hivi kweli hii ni hali halisi
Ya umma
Umma wetu wa watu
Kuuduna
Usiseme
Unyamaze
Wakati unaona hivi hivi
Mtu anajipimia ndani
Ya hifadhi ya karne
Kikataa
A sijui ploti
Kwa uroho wa nafsi
Anaua …yuko tayari
Kuua historia…uhaini mkubwa
Na umma hausemi
Kimya umenyamaza
Hili hata huku niliko
Linaniumiza japo mifupa mitupu


Yale ya langu jicho
Na upande wa sikio
Hayafai
Maana yangekuwa yanafaa
Kama wangekuwa na haya
Au kuona vibaya
Kufikiria wengine…
Mnakula sahani moja
Keshafika upande wako
Anarambaramba
Na wewe unasema
Lako jicho na kidole
Jicho watalitofua
Sikio watalidumua
Na kidole watakikwapua
Kwani hilo la ajabu
Au siri?
Wana roho ngapi
Mwao mikononi walizohujumu
Na haiwashughulishi

Umma lazima useme
Maana mtango unatambaa
Kama ulikuwa masafa
Sasa ujuu yapaa
Na jua litakapotua
Jua la umri wa mamlaka
Kila kitu wamekokozoa
…Yasije yakawa yale ya
Mchezo wa kitoto
Wa nyoka…
Mara keshafika kwako
Unamezwa kwa dakika
Kama hukuwako

Umma lazima useme
Maana akilini nionavyo
Haiingii
Kwa mchezaji kunyongwa
Sababu ya picha yake
Lakini…
Mpiga picha kuonywa
Kwa picha ya mchezaji
Huyo huyo…
Wakati uchi ni ule ule…
Na staha ni ile ile
Na maadili ni yale yale
Mnakwenda wapi nyie waja wa
Dunia mie niliyoiacha

Umma lazima useme
Kwa mkubwa kutania
Maisha ya watu kuchezea
Kwamba “ Maradhi tumeondowa…”
Na watu wakeugua
Na maisha yakepotea
Na kwamba wanamtafuta
Mgonjwa wa dawa
Hata rupia tayari kutoa
…Hakika dharau imekuwa
Ila umma wenu…haya
Waona, wayaona
Ni ya kawaida…
Nguvu ya kuuliza, kuhoji
Imepotea…arijojo
Imekwenda …kama nilivyokwenda
Mimi…


Umma useme leo
Unapoweza kusema
Ujipe nguvu ya kunena
Ungojeapo kesho
Hapatakuwa kalima
Kalima ni leo
Leo ni kalmia
Ya watu ambao
Vya chukuliwa vyao
Zachezewa staha zao
Na hufanyiwa mzaha
Maisha yao
Umma usiposema….

Ally Saleh
Machi 12, 2007

Monday, March 19, 2007

Sisi na wewe nani wa kujitoa kimasomaso?

Mwandishi Maalum, sisi na wewe nani wa kujitoa kimasomaso?

Na Ally Saleh

Haya ni majibu kwa makala ya mtu aliyejitambulisha kama Mwandishi Maalum katika gazeti la Zanzibar Leo la tarehe 11 Machi, 2007, ambayo kiini chake ilikuwa ni kuendeleza mjadala wa kipindi cha Hamza Kasongo Hour kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Channel Ten wiki mbili zilizopita kuzungumzia maisha na kazi za Marehemu Ali Mohammed Nabwa na ambacho, pamoja na wengine, kilimshirikisha mwandishi wa safu hii. Makala hiyo ya toleo namba 1875 katika ukurasa wa 6 iliitwa “Msitumie kifo cha Ali Nabwa kujitoa kimasomaso.” Sasa endelea…


Nimetajwa na Mwandishi Maalum, aliyeandika makala hiyo, ijapo si kwa jina, lakini dunia inaelewa kuwa mimi ni mmoja wa wale walioshiriki mazungumzo katika Channel 10 yenye jina la The Legacy of Ali Nabwa, ambayo ndio yamekuwa kichocheo cha makala hiyo.

Ningeanza kwa kusema Mwandishi Maalum ameutoa ladha mjadala alioukusudia, au kwa watu wa Pwani wanasema katoa upepo kwenye tanga, na ambao ungekuwa mzuri, kwa kuchanganya mambo mawili. Kipindi chenyewe cha The Legacy of Ali Nabwa, kwa upande mmoja, na ghamidha alizonazo, inavyoelekea, kwa Chama cha Upinzani, CUF, kwa upande mwengine.

Mwandishi Maalum amekosea na kwa kweli alianza na wrong premises yaani msingi mbovu kwa kuhusisha kipindi na washiriki wa kipindi na CUF. Hakutaka kabisa kuwaona washiriki wale kwa mtizamo wa kazi zao ila macho yake yametiwa pazia (hooded), kama si nikab, ya siasa.

Inaelekea Mwandishi Maalum ana tabia au ameathiriwa sana na siasa za kugawa watu (divisive politics) na siasa za makundi ya watu (pigeon-holing politics).

Mtu mwenye mitizamo hiyo miwili, kila mtu na kila kitu anakiona katika rangi ambazo ameshaziamua (pre-determined colours) na, hivyo, hana haja ya kushawishiwa na wala kufikiri. Hili ni tatizo kubwa kuwa nalo mtu, maana huwa anazuilika kufikiri na kupanga kwa sababu ya vipingamizi (inhibitions) kama hizo.

Ndio maana Mwandishi Maalum ametupilia mbali kila kilichosemwa na washiriki wa kipindi hicho, na akakosa hoja katika makala yake na kuelekea kwenye siasa za majukwaani za CUF na CCM na mambo ya kifamilia, kama kwamba au anatuonesha kuwa yuko karibu sana na familia ya Nabwa. Pengine kweli.

Laiti angezingatia hoja zilizotolewa, nina hakika angeutajirisha mjadala huu, na asingekuwa na haja ya kujenga hoja zake kwa viguzo vya Qur’an, ambavyo navyo amevichagua kukidhi haja yake.

Pili, Mwandishi Maalum amekosea kwa kuandika katika makala yake vitu vidogo (petty issues) kama vile: “Wengine na mlo wakiutegemea hapo hapo. Wamepungukiwa na mlo na sasa wanalalama wanabaki kuemewa pa kupata chai.”

Hoja hizi za kitoto kuletwa katika mjadala mzito. Zinachusha na zinatoa sura ya namna mwandishi alivyoelemewa na jazba kiasi cha kushindwa kuchuja kinachofaa kuandikwa. Isaidie nini kusema mtu alikuwa anakula kwa fulani katika picha kubwa (bigger picture) ya kujadili maslahi ya nchi au upana wa taaluma na hatma ya mtu?

Au Mwandishi Maalum anatuambia yeye ni msaka tonge na kwa hivyo watu wote anaowaona vile vile? Miongoni mwa kumbukumbu nilizonazo kwa Marehemu Nabwa ni kwamba alikuwa akizungumzia watu aliowaita kwa Kiingereza: “tricky enough to know which side of the bread is well buttered.” Nahofu Mwandishi Maalum asije akawa miongoni mwao.

Au kuanza, katika mfano mwengine: “…waliojitokeza katika kituo kimoja cha TV nchini si masahaba… wasijigambe kuwa wanamuonea uchungu Nabwa. Kwani hilo linaweza kuwafanya wengine walitafsiri vyengine.”

Litafsiriwe vipi vyengine? Yaani kwani tunaogopa kutafsiriwa vyengine? Kuwa kuna kundi linaweza kusemwa ni wapenzi wa Nabwa na wengine sio? Kuwa tuogope kusema tuliyapenda maandishi ya Nabwa na tumeathirika nayo kwa muda wa mwaka tu, tena si zaidi, tuliokaa naye?

Ni kosa kumhusudu mtu na kutaka aenziwe, kama ni hivyo tufute kauli iliyosema 1972, “Kilichokufa na kuzikwa ni kiwiliwili chake, mawazo na fikra zake vipo pale pale…” na mpaka leo tunaadhimisha siku ya kifo cha Abeid Amani Karume, ambaye nae hakuwa mtume? Hivi sote tunampenda Karume?

Na hoja ya Mwandishi Maalum nyengine ni kuwa maadamu watu “hawajamzika akiwa hai,” basi hawana ruhusa ya kujinasibisha naye. Hapa ndipo ninapotaka kumpa funzo Mwandishi Maalum. Funzo lenyewe ni kuwa, kutoa msaada ni kati ya Mwenyeenzi Mungu na mtoaji; na sio kujigamba, au kusifiwa na mtu mwengine kuwa umetoa.

Mwandishi Maalum hivi hakujua ni ria na vibaya hasa kumsifu mtu kuwa amemsimamia maiti, na jee hakuona huko kwa hakika ni kumsimanga maiti na ndiko kutafuta “kujitoa kimasomaso?”

Haielekei kabisa Mwandishi Maalum kuandika: “Tunampongeza Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo kwa uungwana wake na msimamo wake wa kumuuguza Ali Nabwa na kusimamia shughuli zote za “chumba mahututi” hapa Zanzibar hadi Muhimbili.”

Taire, taire Mwandishi Maalum.

Halafu kumbe kule makaburini macho yako au yake yalikuwa yanaduruduru kutizama nani kaenda na nani hajaenda, na pamoja na ujuzi wako wa dini, kwa nukuu nilizoziona, hujui kuwa maziko ni faradhil kifaya yaani ikifanywa na baadhi inatosha na si fardhil ‘ain, ambayo lazima ifanywe na kila mtu mmoja mmoja?

Ukitaka kujua zaidi, Ghassani na mimi hatukuhudhuria kwa sababu tuliamini kumzika Nabwa ni kutoa toleo maalum la gazeti la kumuenzi, na kwa hakika tuliweza katika muda usiozidi saa 24.

Siwezi kuwasemea viongozi wa CUF ambao ulitarajia wahudhurie, na kwa masikitiko yako Mwandishi Maalum, hawakuhudhuria. Lakini umesahau kuwa kuwepo kwa Jussa na Bimani kulitosha kuwakilisha gazeti la DIRA, maana hao wawili ni wakurugenzi wa DIRA.

Na si vyema Mwandishi Maalum akawapa watu picha isiyokuwa ya kweli kuwa wenzake katika Dira walimkimbia Nabwa, na kama asemavyo, “wachache walibakia kwa yao na kwa ajili ya FAHAMU….” Mbona sikuelewi Mwandishi Maalum? Unajua tulivyofungamana? Subiri utatuona!!!

Maana tuliyekuwa karibu naye tulibakia karibu nae. Tulilia naye alipokataliwa uraia. Alituonyesha barua na tukaona saini za watu…wino mweusi, buluu na hata kijani… ambazo zilimdidimiza kuwa asipewe uraia. Sijui iwapo Mwandishi Maalum anajua hayo, ila sisi hatuna haja ya kusema, “ funika kombe…”.

Basi tuliokwenda katika kipindi cha Channel 10 ni mimi, mwaandishi wa habari, na mwandishi wa makala (columnist) Mohammed Ghassani. Tulichokwendea ni kujadili alichokiwacha Nabwa na vipi kinaweza kufaa na kutumika katika jamii, si zaidi si kasoro.

Tabaan, Ali Nabwa kaishi katika jamii, atakuwa ameguswa na mapenzi, chuki na mashakil mengine (love, hatred and intrigues) kama yanavyotukuta wanaadamu wakati wa maisha yetu. Na haya bila ya shaka huwa ndio sehemu ya maumba yanayomuunda (mould) mtu. Na huwezi kumtenga nayo na ndiyo tukayagusia.

Kwetu lile lilikuwa ni zoezi la kitaalum (academic exercise) na hatua ya kukuza uandishi wa habari (enhancing journalism profession) na sio malumbano baina ya vyama vya CUF na CCM. Katika kipindi kile haikutajwa CUF wala CCM kwa njia ya wazi wala ya siri, hata mara moja.

Ila ni watu wa aina ya Mwandishi Maalum peke yao, ndio wanaojifanya wabeba bango la siasa na kuwa wao wana haki ya kumnanga mtu kwa uhusiano wake wa kisiasa, ijapo iwe kwa tafsiri yake tu.

Huu tena si wakati wa kutizama hayo. Maana kama ni kutizama hayo, kuna waandishi wakereketwa kuliko wa vyombo vya serikali ambao wanafika mpaka kuchukua fomu za kugombea kwenye CCM, na bado wanabakishwa kwenye nafasi zao? Jee tusisome makala zao, tusisikilize vipindi vyao au tusiwaheshimu kwa uwezo wao wa kikazi ( professionalism)?

Hivi nikiandika waraka huu, Sauti ya Tanzania Zanzibar inatoa tangazo kutangazia vijana kujiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, lakini, tangazo hilo linasema wazi wazi kuwa wale wataojitokeza wawe ni wana wa CCM tu. Tukuulize Mwandishi Maalum hii kweli ni haki? Hivi kuwa CCM ndio haki na vyama vyengine batil?

Au kwa Mwandishi Maalum kuna ukereketwa mzuri na mbaya, unaokubalika na usiokubalika? Kwa sababu ya kulalia kwake (bias) huko, amejikosesha kuibua mambo mengi yaliozungumzwa kwenye kipindi kile na kuibua mambo yasiohusu kabisa.

Mfano ni pale Mwandishi Maalum anaposema: “ …fungeni midomo yenu, tuna mengi ya kuueleza umma juu ya mapenzi ya CUF kwa wanachama wao ambao si wazaliwa wa Pemba,” na kisha anasema tena sehemu nyengine: “Yanayofanywa sasa kupitia kwa wakereketwa wa CUF ni yale yale tuliyozoea (ya) kupenda kujisifu, ubaguzi wa Upemba na Unguja…”

Tunajua Mwandishi Maalum alikusudia kusema kuwa kama Nabwa angekuwa Mpemba angeshughulikiwa zaidi kwenye mfumo wa CUF, na iwe hivyo, inshallah. Lakini inahusiana nini na mjadala ule wa The Legacy of Ali Nabwa? Ilitajwa popote pale kulaumiwa mtu au taasisi yoyote juu matibabu ya Nabwa?

Naamini Mwandishi Maalum ananijua sana mimi, Ally Saleh, sijui kuhusu Ghassany. Hivi kweli ana moyo na dhati ya kuweza kunihusisha mimi na masuala ya ubaguzi wa Uunguja na Upemba? Hivi hajaweza kunijua kupitia kazi zangu (credentials) kuwa mie niko juu ya vijisiasa viduchu kama hivyo?

Waandishi katika kipindi kile walikiri, ingawa walitofautiana kuhusu kiwango, juu ya kukua kwa uhuru wa vyombo vya habari, maana wangekuwa wajinga wasingesema hivyo (lakini mimi nilizidi), kwa sababu kila mtu anaona hali ilivyobadilika, ila walisema tatizo ni kuwa Serikali ya Zanzibar bado si stahamilivu (tolerant) kwa kukosolewa.

Waandishi walisema juu ya udhalimu wa serikali na kutoheshimu haki za binaadamu. Bado hilo mie nalitamka kwa sababu hakuna duniani serikali ambayo haifanyi dhulma wala iliokuwa mia kwa mia inaheshimu haki za binaadamu, na Zanzibar si mfano bora (not perfect example).

Tuna mengi ya kufanya bado. Mwandishi Maalum namshauri asome ripoti ya Haki za Binaadamu ya Zanzibar 2006 iliyopelekwa Umoja wa Mataifa kama kiambatisho kinachotoka jumuia zisizo za kiserikali, pembezoni mwa ripoti kuu ya Serikali ya Tanzania.

Na ndipo waandishi wakataja mifano. Moja ni la Kurwa Shauri. Pili ni la kufungiwa gazeti la Dira na tatu ni kupokwa urai wa Ali Nabwa. Jengine ni juu ya jengo la ZSTC kuaminika kupewa ama familia au watoto wa Rais wa Zanzibar, Amani Karume, jambo ambalo huko nyuma ndio chanzo cha kufungiwa Dira. Jee hayo si kweli na hayajafanyika, na yanaweza kupita kipimo cha utawala bora (can they go past good governance test?)

Au wakati kuna amri ya Mahakama kuwa Dira inaweza kuomba upya usajili, Waziri anaeshughulika na Habari kusema haiwezekani na kuwa Dira limekufa na halitafufuka, kwenye Baraza la Wawakilishi! Hili nalo linapita kipimo cha utawala bora?

Naona hapa tatizo ni mtu anaeitizama nchi au mambo kwa miwani ya ndani (insiders’ glasses) na hivyo hawezi kuona yaliopo na hali ilivyo nje. Nina wasiwasi Mwandishi Maalum ana miwani ya ndani na, hivyo, anaona kila kinachofanywa na serikali hakina makosa na kama ni hivyo ana mengi ya kujifunza.

Kwetu na kwa wengi, Ali Nabwa alijaaliwa kuwa na kalamu nzuri. Kwetu na kwa wengi, Ali Nabwa kwa urahisi kabisa angewezwa kutamkwa kuwa ni mwandishi habari bora aliyewahi kuzaliwa kutoka Zanzibar. Ni jasiri na, kitu kizuri zaidi, aliishi na kuandika kwa muda mrefu.

Sifa (attributes) hizo ndizo tulizokwenda kuzijadili na vipi tutaweza kuzikuza na kuziendeleza. Ali Nabwa ameacha maandishi kadhaa. Sasa jee vipi yatahifadhiwa, na mambo gani waandishi wajifunze kutoka kwake? Na si waandishi tu; lakini jamii kwa ujumla ambayo aliifungua macho kwa mengi aliyoandika ambayo wengine walikuwa nayo lakini hawakupata fursa au waliogopa kuandika.

Lakini Mwandishi Maalum anaelekea ni bingwa wa kejeli (master of cynism) kwa vibwagizo kadhaa alivyovitoa kama vile aliposema: “Tuliowaona ni wale wapiga cherewa za CUF, waimbaji hasa hawakuja kumsitiri mwenzao,” (msisitizo ni wangu).

Pia anazua mambo ambayo Ghassany wala mimi hatukusema. Yeye anasema: “Leo vyereje waibuke watu kuilaumu Serikali eti imechangia kifo cha Ali Nabwa kwa sababu ya kulifungia gazeti la Dira?”

Mwandishi Maalum tafadhali sema lililosemwa, halafu kwa hilo jibu hayo mapigo unayotaka. Kwa ajili ya rekodi, kilichosemwa, na bado ambacho tunaendelea kukisema, ni kuwa afya ya Nabwa ilidhoofika baada ya kusumbuliwa kutokana na suala la uraia wake.

Ama hayo mengine aliyosema Mwandishi Maalum kama vile, hajapitiwa kuulizwa hali, au watu kushindwa kuchangisha fedha ndogo za matibabu, mie sina haja nayo kwa madhumuni ya makala hii, maana si ya msingi.

Ila napenda kumjulisha mimi sio katika hao asemao: “simba amekwisha kufa nyinyi mjipake damu?” Sina haja ya kujipaka damu ya simba aliyekufa na ndio maana nikasema katika Chanel 10 kuwa sina uwezo wa kuvaa viatu vya Ali Nabwa, lakini ieleweke huyo simba nimekaa naye na niliweza kuona jinsi kina tembo, kifaru, chui na kiboko walivyokuwa wakimuogopa, na ndipo wakamuwinda mpaka wakamtia mtegoni.

Napenda kumalizia kwa kumuambia Mwandishi Maalum kuwa sisi “waungwana chipukizi” tumekusikia, lakini tunakuhakikishia hatuna maslahi yoyote tunapomzungumzia Nabwa zaidi ya mapenzi yetu kwake. Mimi nina jina la kutosha ingawa si kubwa kama la Nabwa na wala sina cha kujitolea kimasomaso kwayo.